Get New DJ Mixes
MUSIC

Ukweli Maiti ya Corona Kuambukiza Corona

Ukweli Maiti ya Corona Kuambukiza Corona

JANGA la mlipuko wa maambukizi ya Virusi vya Corona vinavyosababisha Ugonjwa wa COVID-19, limemfanya binadamu kushuhudia mambo ya kutisha mno.

Binadamu wa sasa ameshuhudia picha za kifo cha binadamu mwenzake ambaye hata kama ni ndugu, jamaa, rafiki au mpendwa wake, haruhusiwi kumuombolezea au kumpa heshima yake ya mwisho kama ilivyozoeleka.

Picha hizo zimesababisha hofu kwa binadamu anayeziona, namna ambavyo mpendwa wake aliyekufa kwa Corona anavyopumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.

Hofu imesambaa duniani kote kabla ya kifo na baada ya kifo ambapo maiti ya Corona inaogopwa mno kwa madai ya kwamba, inaambukiza virusi hivyo.

MAITI YA CORONA INAWEZA KUAMBUKIZA CORONA?

Swali kuu la msingi kwenye makala haya ni je, maiti ya Corona inaweza kuambukiza Corona (COVID-19) na je, ni salama kushiriki mazishi yake?

Majibu; Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema; watu wanaobeba jeneza lenye maiti ya mtu aliyekufa kwa Corona, wanapaswa kuvaa mavazi ya kujikinga mno na virusi hivyo hatari.

Shirika hilo linasema, endapo tahadhari muhimu zitachukuliwa, basi hakuna sababu ya kuogopa.

Maelezo ya kina yanasema, virusi hivi huenezwa zaidi kwa njia ya cheche za mate au ute unaotoka kwa binadamu. Kwa mfano; wakati tunapozungumza, kupiga chafya au kukohoa.

Hata hivyo, wataalam wanasema kuwa, virusi hivi vinaweza kuishi kwa hadi siku kadhaa kwenye vitu fulani vigumu na hata maiti.

“Hakuna ushahidi kuhusu hali ya maambukizi kutoka kwa binadamu aliyekufa kwenda kwa binadamu aliye hai,” anasema William Adu-Krow ambaye ni Msemaji wa Shirika la Afya la Marekani.

VIRUSI VINAWEZA KUISHI KWENYE MAITI?

Je, virusi hivi vinaweza kuishi kwenye maiti?

Majibu; kwa mujibu wa wataalam, maiti inaweza kuhifadhi virusi katika viungo vya mwili, kwa hiyo tahadhari zinahitajika wakati wa kuishughulikia.

 “Haimaanishi kwamba, kwa sababu tunasema haiwezi kuambukiza na unampenda mpendwa wako aliyekufa kwa Corona, hivyo unaweza kumbusu au kufanya chochote cha aina hiyo,” anasema mtaalam huyo.

Anaendelea kusema kuwa, maiti iliyotokana na ugonjwa mbaya wa mfumo wa kupumua, inaweza kuwa na virusi hai katika mapafu na viungo vingine vya mwili.

Anaongeza kuwa, virusi hivi vinaweza kutolewa wakati wa upasuaji wa uchunguzi wa mwili, ambapo vifaa vya kimatibabu hutumiwa. Au wakati wa kuosha ndani ya mwili.

NINI CHA KUFANYA?

Nini cha kufanya? Majibu; kama una ndugu, jamaa au rafiki aliyekufa kwa Corona, yafaa maiti yake kuandaliwa kwa mazishi au kuchomwa na mtu mwenye mafunzo yanayofaa na wataalam waliojikinga.

Hata hivyo, sote tunafahamu kuwa, mazishi yamepigwa marufuku au kuwa na masharti makali kote duniani kutokana na Corona.

Kumekuwa na kanuni za kutosogeleana, mazishi yamepigwa marufuku katika nchi kadhaa na baadhi bado zinaruhusu, lakini yanahudhuriwa na idadi ndogo sana ya watu.

WHO inasema wanafamilia na marafiki wa marehemu, wanaweza kutazama mwili wakati wa mazishi, ilimradi wazingatie masharti fulani yaliyowekwa.

“Hawapaswi kugusa au kubusu mwili na wanapaswa kunawa mikono yao vema kwa sabuni na maji baada ya kuutazama mwili, hatua za kukaa mbali na mwili zinapaswa kuzingatiwa (walau kuwe na umbali wa mita moja,” unasema mwongozo wa WHO.

NANI HAPASWI KUHUDHURIA MAZISHI?

Maagizo mengine yanasema, watu wenye dalili za magonjwa ya mfumo wa kupumua, hawapaswi kuhudhuria mazishi au iwapo watalazimika, wanapaswa kuvaa barakoa kuzuia kusambaa kwa maambukizi.

Pia kundi lingine lisilopaswa kuhudhuria mazishi ya maiti ya Corona ni watoto, watu wazima wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na wenye kinga dhaifu ya mwili.

KUZIKA AU KUCHOMA, KIPI SAHIHI?

Majibu; WHO inasema kuzika au kuchoma maiti ya Corona, vyote vinakubalika.

“Ni imani ya kawaida kwamba watu ambao wamekufa kutokana na magonjwa yanayoambukiza, wanapaswa kuchomwa, lakini hilo si kweli.

“Kuchoma maiti ni suala la utamaduni unaochaguliwa na jamii husika,” inasema WHO na kuendelea kusisitiza watu kuchukua tahadhari kujikinga na janga hili linalotishia uhai wa binadamu hapa duniani.